highlights


Reports and Policies

News and Events

Hotuba ya Rais Kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 2007

Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Dodoma, tarehe 16 Juni, 2007

Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto;

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

Waheshimiwa Mawaziri;

Waheshimiwa Wabunge;

Watoto Wetu Mliopo Hapa;

Wageni Waalikwa.

Mabibi na Mabwana.Ndugu Wananchi;

Kwanza kabisa napenda kuelezea furaha kubwa niliyonayo kwa kualikwa kwangu hapa siku ya leo. Nimefurahi sana kwa kupewa fursa hii ya kushiriki kwenye maadhimisho haya ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu. Nikiwa kama mzazi na mlezi nimefarijika sana kukutana nanyi watoto, tena watoto wenye nyuso za furaha na matumaini, katika sherehe hizi hapa Dodoma.

Nawashukuru viongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na watoto wote nchini kwa jumla kwa heshima hii kubwa mliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi. Kwenu nyote nasema asanteni sana.

Aidha, napenda kuwapongeza viongozi na wananchi wa mkoa huu wa Dodoma pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuandaa sherehe hizi. Sote tunatambua uzito na ugumu wa kuandaa sherehe kama hii, hasa pale inapowajumuisha watoto. Si kazi rahisi hata kidogo. Hivyo wamefanya kazi kubwa na inayoonekana. Kwa niaba ya waalikwa wote tulioko hapa, nawapongeza sana kwa kufanikisha sherehe hizi.

Nawapongeza pia Wajumbe wa Baraza la Watoto kwa risala yao nzuri na ya kusisimua iliyosheheni ujumbe mzito kwetu sote. Napenda kuwaahidi kuwa tutayafanyia kazi mambo yote mliyotueleza. Napenda pia kuitumia nafasi hii kuwapongeza watoto wote waliotunukiwa zawadi siku ya leo. Naomba zawadi mlizozipata ziwe ni chachu ya kuwasukuma kupata mafanikio makubwa zaidi katika siku zijazo. Wale ambao hawakutunukiwa leo wasikate tamaa bali waendelee kujitahidi ili nao mwakani waweze kutunukiwa zawadi kama wenzao.

Ndugu Wananchi;

Baada ya shukrani na pongezi hizo sasa napenda kutumia nafasi hii kusema mambo machache yanayohusu maendeleo ya watoto wetu hapa nchini. Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 idadi ya watoto nchini ilikadiriwa kufikia 19,583,922 mwaka wa jana 2006. Kati yao wavulana ni 9,833,919 na wasichana 9,750,003. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 51 ya watu wote nchini.

Takwimu hizi ni muhimu sana. Kwanza zinaonyesha kwamba watoto ndiyo walio wengi zaidi katika idadi ya watu wa Watanzania.

Kwa maana hiyo watoto wanastahili kusikilizwa, kuendelezwa na kuhudumiwa ipasavyo na wazazi wao ili waweze kukua na kuishi katika mazingira mazuri na salama. Wanahitaji kulindwa dhidi ya maradhi, ukatili, uonevu na unyanyasaji. Wanahitaji pia kuendelezwa kwa kupatiwa elimu bora kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu.

- Ukatili wa kwanza ni ule wa kunyimwa haki ya kuzaliwa kwa kutoa mimba. Kina mama wapeni watoto haki ya kuzaliwa. Najua wapo wenzetu wanaoamini ni haki ya mama kuchagua kuzaa au kutokuzaa. Lakini katika kutumia haki hiyo nashauri wachague kutokupata mimba na siyo kupata mimba halafu kuitoa ni kumnyima mtoto haki ya kuishi.
- Ukatili mwingine ni kuwanyima haki ya kusoma kwa kuwapa mimba watoto wadogo. Wenzangu ni aibu.
- Ukatili mwingine tunaowafanyia watoto ni kuwanyima fursa ya kucheza hasa mijini. Maeneo yote ya wazi watoto wangeweza kucheza tumeyagawa kwa matajiri au hatujali kabisa yawepo.

Tukifanya hivyo, tutakuwa tumewajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye. Pia tutakuwa tumewajengea uwezo wa kutosha utakaowawezesha kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Hivyo tunapoadhimisha siku hii adhimu katika bara letu, hatuna budi kuangalia upya mtazamo wetu kama wazazi, walezi na jamii kwa jumla kuhusu majukumu yetu kwa malezi na makuzi ya watoto hapa nchini. Baadhi ya majukumu hayo tayari tumekumbushwa na watoto katika risala yao waliyoisoma hapa hivi punde. Naomba ndugu zangu sote tuyazingatie.

Ndugu Wananchi;

Mheshimiwa Waziri katika maelezo yake ameeleza matatizo mbalimbali yanayowakabili watoto wetu. Nisingependa kuyarudia tena matatizo hayo. Niseme tu kwamba katika siku za nyuma niliwahi kuwataka wadau mbalimbali kukaa pamoja na kuandaa mipango endelevu ya kuwalea na kuwasaidia watoto. Nilisisitiza haja na umuhimu wa jamii yetu kuwasaidia kwa hali na mali watoto yatima na wale walio katika mazingira magumu ili nao waishi maisha ya furaha na upendo kama walivyo watoto wengine.

Nafurahi kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iko mbioni kukamilisha mpango wa uanzishaji wa mfuko wa kuwasaidia watoto yatima na walio katika mazingira magumu. Nawaomba wale wote wanaohusika na kuandaa mpango huo waongeze kasi ili kazi hiyo ikamilike mapema. Nia yetu ni kuwa na mfuko utakaotumika katika kuwahudumia watoto hawa ambao wengi wao wanaishi katika mazingira magumu na idadi yao inazidi kuongezeka siku hadi siku.

Napenda kutumia fursa hii kutambua na kutoa pongezi za dhati kwa mchango mkubwa unaotolewa na mashirika ya kidini na asasi zisizo za kiserikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Wanafanya kazi nzuri na ya kusifika. Dhamira yetu serikalini ni kuendelea kushirikiana na mashirika na asasi hizo katika kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapata malezi na makuzi bora ambayo ni haki yao ya msingi.

Ndugu Wananchi;

Jukumu la kulea, kutunza na kuwaendeleza watoto ni letu sote. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wanakua na kuishi katika mazingira yaliyo bora na salama. Hata hivyo wajibu wa kwanza upo mikononi mwa wazazi, yaani baba na mama. Hawa ndiyo nguzo kubwa ya maisha ya watoto wetu. Wakiwa wazazi wanao wajibu mkubwa na wa kipekee wa kuhakikisha kuwa watoto wanaowazaa wanapata haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na mapenzi ya wazazi ili kuwawezesha kukua katika hali ya upendo na furaha.

Pili, lipo pia jukumu la familia, yaani ndugu wa karibu na wazazi wa mtoto. Kundi hili linajumuisha watu kama vile shangazi, mjomba, babu, bibi na ndugu wengine. Hawa wote wanao wajibu wa kumlea mtoto vizuri hasa pale inapotokea wazazi wa mtoto hawana uwezo mkubwa, au kifo cha mmoja wa wazazi au wazazi wote wawili. Familia ione soo kumuacha mtoto wa ndugu yao anateseka au kuhangaika wakati wao wapo. Familia pia ni muhimu sana katika kujenga maadili mema ya watoto wetu na kuwawezesha kuwa raia wema hapo baadaye.

Tatu, jukumu lingine ni la jamii, yaani watu wanaoishi karibu na wazazi wa mtoto, kwa mfano kijijini. Jamii inao wajibu wa jumla wa malezi na makuzi ya mtoto hata kama hawana uhusiano wa damu na mtoto huyo. Jukumu hili katika mazingira ya nchi zetu za Kiafrika ndiyo asili yetu na mila yetu.

Ndiyo utu wa Mwafrika huo. Mila zetu zinamruhusu mtu mzima kumkemea au kumuasa mtoto wa jirani yake au hata mtoto wa mtu asiyemfahamu, pale anapomwona anafanya vitendo vinavyokinzana na maadili mema. Utamaduni huu ni mzuri na una manufaa makubwa kwa jamii yetu. Naomba kwa pamoja tuuimarishe na tuuendeleze. Najua siku hizi kuna matatizo hasa mijini lakini tusirudi nyuma. Tuusisitize. Manufaa yake ni makubwa kuliko hasara.

Lakini jukumu la majirani haliishii hapo tu. Majirani na watu wengine katika jamii wanao pia wajibu wa kutoa misaada kwa watoto wanaokabiliwa na matatizo maalum. Misaada hiyo ni pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola pale inapolazimu ili kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya watu katika jamii yetu.

Utamaduni huu pia naomba tuuendeleze ili kuwabana watu wachache wenye tabia mbaya ya kuwanyanyasa na kuwafanyia watoto wetu vitendo vya ukatili. Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wenye tabia hii mbovu ili kulinda afya na maisha ya watoto. Napenda kusisitiza kuwa katu hatutawaacha waendelee kufanya vitendo hivyo viovu dhidi ya watoto wetu. Kila mara tutahakikisha kuwa wanafikishwa mbele ya sheria na wanaadhibiwa ipasavyo.

Aidha, napenda kuwasihi Watanzania wenzangu kuachana na fikra na mila potofu kuhusu maendeleo ya mtoto na hasa mtoto wa kike. Naomba tuachane na vitendo vyote vinavyodumaza maendeleo ya watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kutowapeleka shule na kuwaozesha wasichana katika umri mdogo, jambo ambalo pia linahatarisha maisha yao.

Mila na desturi za aina hii ambazo bado zinashamiri kwenye baadhi ya makabila yetu zimepitwa na wakati na ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na mustakabali wa nchi yetu. Hivyo tushirikiane kwa pamoja katika kupiga vita mila hizo ili kuwajengea watoto wetu mazingira bora ya maisha na kuwapa fursa ya kuendeleza vipaji vyao walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kufanya vinginevyo ni kuwanyima haki watoto na kudumaza maendeleo yao, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa;

Nimeambiwa kuwa kaulimbiu ya maadhimisho haya mwaka huu ni Afya Bora kwa Mtoto ni Msingi wa Maendeleo. Mimi nakubaliana na kaulimbiu hiyo kwa asilimia zote. Kwani ni jambo lililo wazi kuwa maendeleo ya nchi yetu kwa kiwango fulani yanategemea sana hali za afya za watoto wetu ambao ndio nguvukazi ya baadaye. Tukiimarisha afya za watoto wetu tutawajengea makuzi mazuri ya kimwili na kiakili na hivyo kuwaandaa kuwa nguvukazi ya kutegemewa na taifa letu katika siku za usoni.

Wataalamu wanatueleza kwamba ili mtoto aweze kukua vizuri, matunzo yake katika kipindi cha ujauzito wa mama yana uhusiano mkubwa na afya yake ya kimwili na kiakili atakapozaliwa. Serikali kwa kutambua hili imekuwa ikitilia mkazo mkubwa katika suala zima la afya ya mama na mtoto.

Moja ya hatua tulizozichukua ni kuhakikisha kwamba kupitia Sera ya Taifa ya Afya, watoto wote chini ya miaka 5 na akina mama wajawazito wanapatiwa chanjo na matibabu bure. Aidha, hivi sasa tunaendelea na uimarishaji wa mkakati wa kupunguza vifo vya watoto na akina mama wajawazito. Nafurahi kusema kwamba tayari dalili za mafanikio zinaanza kuonekana kwa upande wa vifo vya watoto. Idadi ya vifo vya watoto nchini imekuwa ikipungua. Kwa mfano, idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano ilipungua kutoka 147 kwa kila watoto 1,000 mwaka 1999 hadi kufikia vifo 112 kwa kila watoto 1,000 mwaka 2005. Si punguzo kubwa sana la kujivunia, lakini inatia moyo.

Lengo letu ni kuendelea kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi kufikia vifo 79 kwa kila watoto 1,000 ifikapo mwaka 2010. Aidha, tumekusudia pia kufikia Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa yanayotuhitaji kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili ifikapo mwaka 2015. Naamini tunao uwezo wa kufikia lengo hilo. Kinachotakiwa ni kuongeza kasi ya jitihada zetu na kuimarisha ushirikiano wa kila mmoja wetu katika kuboresha hali za maisha yetu na ya watoto wetu.

Kwa upande wa akina mama wajawazito hali bado siyo nzuri sana. Bado kati ya akina mama wajawazito laki moja 578 hufariki kwa matatizo ya uzazi. Idadi hii ni kubwa sana na ni changamoto kwetu sote. Inatubidi tuongeze kasi ya mapambano yetu dhidi ya tatizo hili ili tuweze kufikia Malengo ya Milenia yanayotutaka kupunguza kwa robo tatu vifo vya kina mama wajawazito ifikapo 2015. Mimi naamini, kama ilivyo kwa watoto, tunao uwezo wa kufikia pia lengo hili linalohusu akina mama wajawazito. Tunachotakiwa kufanya ni kujipanga vizuri.

Ndugu Wananchi;

Katika kuimarisha jitihada zetu za kupambana na tatizo hili, hivi karibuni tunatarajia kuzindua mpango kamambe wa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati mijini na vijijini hapa nchini. Mpango huu ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, unalenga katika kupeleka huduma za afya karibu zaidi na wananchi. Tunataka wananchi wasitembee zaidi ya kilomita tano kutafuta huduma ya afya.

Mimi na wenzangu serikalini tunaamini kuwa tukifanikiwa katika hili tutakuwa tumejijengea uwezo mkubwa na mazingira mazuri zaidi ya kuokoa maisha ya watoto wetu hasa wale walioko vijijini ambako kwa sasa upatikanaji wa huduma za afya siyo wa kuridhisha sana.

Aidha, upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi utawawezesha akina mama wajawazito wengi zaidi kujifungua chini ya uangalizi wa manesi na waganga. Hali hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo kwa mtoto na mama vinavyosababishwa na matatizo mbalimbali ya uzazi. Hivi sasa asilimia 53 ya watoto wote nchini wanazalishwa na wakunga wa jadi nje ya mfumo wetu wa huduma ya afya. Ni asilimia 47 tu ya watoto nchini ndio wanaozaliwa kwenye hospitali, zahanati na vito vya afya.

Kwa kutambua ukweli kuwa kwa miaka kadhaa ijayo wakunga wa jadi wataendelea kutegemewa, Serikali imedhamiria kuwapa mafunzo na vifaa bora vya kazi. Hii itawaongezea uwezo, ujuzi na maarifa zaidi ya kuhudumia kina mama wazazi.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa;

Naomba nimalize kama nilivyoanza. Nawashukuru tena waandaaji na watoto wote kwa kunialika na kwa kufanikisha maadhimisho haya ya Mtoto wa Afrika. Nawasihi Watanzania wenzangu tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha maendeleo na ustawi wa watoto wetu.

Watoto ndiyo hazina ya Taifa letu. Watoto ndiyo nguvukazi ya baadaye. Watoto ndiyo Taifa letu la kesho. Naomba tuwapende, tuwathamini na tuwaendeleze. Tufanye hivyo kwa kutambua kuwa kuwalea watoto wetu ndio wajibu wetu wa msingi kwao kama wazazi na jamii. Naamini hili linawezekana. Kila mmoja hana budi kutimiza wajibu wake.

Asanteni kwa kunisikiliza.