highlights


Reports and Policies

News and Events

Hotuba ya Rais kwenye Uzinduzi wa Benki ya Wanawake Tanzania

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE UZINDUZI WA BENKI YA WANAWAKE DAR-ES-SALAAM, TANZANIA

Mheshimiwa Margaret Sitta, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto;

Waheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo- WAMA; Mama Sitti na Mama Khadija;

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri mliopo hapa;

Dr. Lucy Nkya, Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto;

Mheshimiwa William Lukuvi, (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Bibi Mariam Mwaffisi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto;

Bwana Daniel Ole Sumayan, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Wanawake Tanzania;

Waheshimiwa Wabunge;

Wajumbe wa Bodi ya Benki ya Wanawake Tanzania;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mbwana:

Utangulizi

Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na hasa bahati ya kushuhudia tukio hili la kihistoria la uzinduzi wa Benki ya Wanawake Tanzania. Nakushukuru sana Mheshimiwa Margareth Sitta, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, na uongozi wa Benki ya Wanawake Tanzania kwa kunialika kushiriki katika shughuli hii adhimu.

”Hayawi hayawi leo yamekuwa.” ”Walisema hawapati mbona wamepata”? Hayo ndiyo maneno ninayopenda kuanza nayo katika hotuba yangu ya ufunguzi wa Benki ya Wanawake Tanzania. Maneno hayo yanaelezea kwa ufasaha na usahihi ukweli kwamba leo ni siku ya aina yake katika historia ya nchi yetu na hasa kwa maendeleo ya wanawake hapa nchini. Ni siku ambayo ndoto ya miaka mingi ya wanawake wa Tanzania ambayo ilionekana kama haiwezekani hatimaye imewezekana. Tumekusanyika hapa kuwa shuhuda wa kutimia kwa ndoto hii.

Kilio cha Siku Nyingi cha Wanawake

Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kuwepo kwa benki ya wanawake nchini ni maombi na kilio cha wanawake wa nchi yetu tangu uhuru. Ni kilio kilichotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake tangu wakati wa TANU na hata baada ya CCM kuzaliwa. Ni kilio cha Bibi Titi Mohamed na Mama Sofia Kawawa wakati wa uhai wao wakiwa Wenyeviti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Ni kilio cha Mheshimiwa Anna Abdallah wakati akiwa Mwenyekiti wa UWT na ni kilio cha Mheshimiwa Sophia
Simba akiwa Mwenyekiti wa sasa wa UWT. Hakuna Mwenyekiti wa UWT ambaye hakusemea jambo hili. Ni kilio cha wanachama wao na wanawake wote nchini.

Kilio hicho cha wanawake wa Tanzania kilifikishwa kwa viongozi wote Wakuu wa nchi yetu tangu uhuru. Kilitolewa kwa Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere, kwa Rais wa Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, kwa Rais wa Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na hata kwangu pia. Kwetu sisi viongozi wote maombi yalipofikishwa, ahadi yetu ilikuwa ni kuyafanyia kazi. Kila mmoja wetu kwa wakati wake alichukua hatua mbalimbali na sasa tumehitimisha.

Ndugu Wananchi;

Waswahili wana misemo miwili ambayo napenda kuinukuu; ”safari ni hatua” na ”kila jambo kwa wakati wake”. Hatimaye wakati umetimia kwa jambo hili kukamilika kama tunavyoshuhudia leo. Hatuna budi kumshukuru kwa namna ya pekee Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwa maono yake ya mbali na uamuzi wake wa busara na kishujaa wa kukubali uanzishaji wa Benki ya Wanawake uwemo katika Ilani za Uchaguzi za CCM za mwaka 2000 na ile ya 2005. Ibara ya 120(g) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 inaagiza kuwa: ”Kukamilisha taratibu na hatimaye kuunda Benki ya Wanawake”. Nasema ulikuwa ni uamuzi wa kishujaa kwa sababu kukubali jambo hili ambalo kwa miaka ya nyuma halikuweza kutekelezwa liwe ahadi bayana ya Chama Cha Mapinduzi kunahitaji moyo wa ujasiri na kuthubutu. Nampongeza kwa uwezo wake wa kuona mbali na imani yake kwamba katika awamu ya nne ya uongozi wa nchi yetu jambo hili litawezekana. Na kweli limewezekana. Naomba kwa mara nyingine tena tumtambue na kumpongeza Mzee wetu Benjamin William Mkapa.

Ndugu Wananchi;

Napenda kuitumia nafasi hii kuwatambua na kuwashukuru wenzangu wote katika Serikali ninayoiongoza kwa utendaji kazi wao mzuri uliowezesha ndoto ya wanawake na ya wananchi wetu wa Tanzania kutimia. Niruhusuni niwataje watu wanne kwa niaba ya wenzao wote waliohusika, moja kwa moja, katika kufanikisha kuwepo kwa Benki ya Wanawake Tanzania tunayosherehekea uzinduzi wake leo. Wawili wa kwanza ni kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Watoto, yaani Mheshimiwa Sophia Simba aliyekuwa Waziri wangu wa kwanza wa Wizara hiyo na Mheshimiwa Margareth Sitta ambaye ndiye Waziri wa sasa. Waziri Sophia Simba ndiye aliyepanda mbegu na Waziri Margareth Sitta ndiye aliyemwagilia maji mpaka mti ukakua, ukakomaa na kutoa matunda tunayoyachuma sasa.

Wawili wengine ni Mheshimiwa Zakhia Meghji aliyekuwa Waziri wangu wa kwanza wa Fedha na Mheshimiwa Mustapha Mkullo, Waziri wa sasa. Mheshimiwa Zakhia Meghji aliunga mkono uamuzi wangu kuwa Serikali ichangie fedha zake kuwezesha Benki hii kuanza. Wakati ule Waziri Sophia Simba alikuwa ameanzisha mchango wa kuanzisha Benki hiyo na makusanyo hayakuwa yanaenda kwa kasi iliyoniridhisha. Nilipomwambia Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Zakhia Meghji wakati ule kuwa Serikali itenge pesa kwenye bajeti yake kuchangia Benki ya Wanawake hakusita, akakubali na kuanzisha mchakato. Mheshimiwa Mustapha Mkullo amekuja kuukamilisha mchakato huo na matokeo yake ni Serikali kutoa shilingi bilioni 2.9 na kuwezesha kuwepo kwa Benki hii hivi leo. Mchango huu siyo mwisho, Serikali itaendelea kuchangia mtaji wa benki hii kadri itavyowezekana. Wakati tukiwashukuru viongozi hao wa kisiasa hatuna budi kuwashukuru watendaji mbalimbali waliokuwa chini yao kwa kazi yao nzuri iliyowezesha mambo kukamilika vizuri kama tunavyoshuhudia leo.

Umuhimu wa Kuanzisha Benki ya Wanawake

Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Tanzania ni kitendo cha kihistoria kinachotambua nafasi ya mwanamke nchini na kumtendea haki. Wanawake ni wengi kuliko wanaume hapa nchini. Ni asilimia 50.8 ya watu wote Watanzania. Hivyo basi wanaume ni asilimia 49.2. Wanawake ndiyo wanaobeba mzigo mkubwa wa kazi ya uzalishaji mali mashambani pamoja na ile ya kutunza familia nyumbani. Lakini, wanawake hao wanaotoa mchango mkubwa sana kwa uchumi wa familia na jamii kwa jumla, wengi wao ni maskini. Ukweli ni kwamba, hapa nchini pamoja na wananchi wengi kuwa maskini (asilimia 33.3 kwa takwimu za 2007) lakini kati yao wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume.

Wanawake wapo katika hali hiyo kwa sababu ya mazingira maalum wanayoishi nayo. Baadhi ya mila na desturi za makabila yetu mengi zinamfanya mwanamke awe hivyo. Bahati mbaya pia baadhi ya sheria zetu zinaendeleza na kuendekeza unyanyasaji na ukandamizaji wa wanawake. Kiserikali tumezirekebisha baadhi ya sheria hizo na kazi bado inaendelea. Kwa upande wa mila na desturi baadhi ya sheria tulizotunga zimesaidia kuzirekebisha na tutakazotunga siku za usoni zitasaidia zaidi. Hata hivyo, hatuna budi kuendeleza juhudi katika jamii zetu na makabila yetu nchini za kubadili mila na desturi zinazoathiri vibaya haki na maendeleo ya wanawake na kuwafanya wengi wao kuwa maskini. Pamoja na hayo ambayo mafanikio yake yameanza kuonekana bado imekuwepo na bado ipo haja ya kuwepo mipango ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa mikopo ili waweze kujinasua kutoka katika lindi la umaskini. Kukosekana kwa asasi ya fedha yenye uwezo na mtaji mkubwa wa kuwawezesha wanawake kupata mikopo mikubwa zaidi ambayo wataitumia kama mitaji ya kuendeleza shughuli zao kiuchumi umekuwa upungufu mkubwa.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Hivyo basi kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Tanzania ni hatua muafaka ya kutatua tatizo hili katika dhamira azizi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Ni ushahidi mwingine kwamba Serikali yetu inawajali wanawake wa Tanzania na inayo dhamira ya dhati ya kuinua hali zao za maisha. Kuwepo kwa Benki hii na kuanza kazi rasmi kunatoa fursa kwa wanawake wa Tanzania kutumia huduma zake kujiletea maendeleo na kuondokana na umaskini. Nimefarijika sana kusikia kwamba wanawake wengi na wanaume pia wamejitokeza kutumia huduma za Benki hii tangu ifungue milango yake tarehe 28 Julai, 2009. Ni matumaini yangu kwamba, watu wengi zaidi na hasa wanawake watajitokeza kufungua akaunti katika Benki hii. Natoa wito kwa wanawake wote Tanzania, ambao benki hii ipo kwa ajili yao, wawe mstari wa mbele kufungua akaunti na kununua hisa. Wakifanya hivyo watakuwa wamiliki halisi wa benki na kufaidi zaidi matunda yake. Hivyo basi, napenda kusisitiza umuhimu wa wanawake wa Tanzania kujitokeza kwa wingi na kuwa mstari wa mbele katika kuistawisha Benki yao. Lazima muonekane mkifanya hivyo, vinginevyo vilio vyenu vya huko nyuma vitakuwa havieleweki na juhudi zetu wengine zitakuwa sawa na kilio nyikani. Zitakuwa zimepotea bure. Siamini kuwa mtaacha hayo yatokee.

Pamoja na kusema hayo kuhusu wanawake, ni vizuri nikasisitiza ukweli kwamba benki hii ipo kwa ajili ya watu wote: wanawake na wanaume. Hivyo napenda kutumia nafasi hii pia kutoa wito kwa wanaume wenzangu kote nchini kujitokeza kufungua akaunti na kununua hisa katika Benki hii. Lazima tujitokeze kuwaunga mkono mama zetu, wake zetu, dada zetu na mabinti zetu. Hatuna budi kukumbuka ule msemo maarufu kuwa ‘’kila kwenye mwanamke aliyefanikiwa, nyuma yake kuna mwanaume anayejali.’’ Sasa ni wakati wetu wanaume kuonyesha tunajali kwa kusaidia Benki ya Wanawake Tanzania istawi na kufanikiwa katika malengo yake.

Mchango wa wanaume ni muhimu kama watu wenye wajibu kwa maendeleo ya wanawake kama vile ambavyo wanawake huchangia kwa maendeleo ya wanaume. Vile vile, ni ukweli ulio wazi kwamba katika jamii wanaume ndiyo wenye uwezo mkubwa kiuchumi kuliko wanawake. Hivyo basi, lazima wanaume wawe mstari wa mbele kununua hisa na kufungua akaunti katika Benki ya Wanawake. Pia wanaume wasaidie kuwashawishi wanaume wenzao, marafiki zao, wake zao, watoto wao na ndugu zao wanunue hisa na kufungua akaunti zao katika Benki hii. Aidha, niwaombe wafanyabiashara na makampuni makubwa na madogo nao kufanya hivyo hivyo. Ningefurahi sana pia kama asasi za Serikali na zisizo za kiserikali nazo zikafungua akaunti katika Benki hii. Kama haya yote yatafanyika Benki ya Wanawake Tanzania itapata mafanikio makubwa tunayoyatarajia sote katika muda usiokuwa mrefu.

Tujenge Benki

Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Wakati huu tunapozindua rasmi Benki ya Wanawake Tanzania, napenda pia kuwakumbusha msemo ambao wanawake wanaujua sana maana yake. Nao si mwingine bali ni ule usemao ‘’kuzaa si kazi, kazi kulea”. Ni kweli tumehangaika sana kwa miaka mingi, tangu uhuru, mpaka leo tunapopata bahati ya kuwa na hii benki. Haikuwezekana huko nyuma sasa tumeweza. Lakini, kazi kubwa inaanza sasa. Kazi hiyo si nyingine bali ile ya kuhakikisha kuwa Benki hii inajengeka na inaendeshwa vizuri ili kiwe ni chombo cha fedha kilicho kizuri, imara, kinachojengeka, kukua na kuendeshwa kwa kuzingatia misingi stahiki ya weledi wa kibenki. Haya yote yatapatikana kwa kuwa na menejimenti nzuri inayojua vizuri kazi yake ya uendeshaji na kutambua vyema wajibu wake na kuutekeleza ipasavyo kwa kuzingatia kanuni za weledi wa shughuli za kibenki. Pia kwa kuwa na watumishi wenye ujuzi wa kutosha wa kazi za kibenki, wachapa kazi hodari, waaminifu na waadilifu.

Mfanikio ya benki hii yatategemea kuwa na Bodi ya Wakurugenzi nzuri inayotambua vyema wajibu wake wa uongozi wa benki. Bodi ambayo wajumbe wake ni watu makini, wabunifu, waaminifu na waadilifu. Mambo haya ni sharti muhimu sana kwa kukua na kuimarika kwa Benki yetu hii sasa, miaka mingi ijayo na kwa wakati wote wa uhai wake. Pengine, haya niyasemayo sasa ni muhimu zaidi hapa mwanzoni kwani ukianza vizuri unajihakikishia mafanikio mazuri baadae na hatma njema. Nayasema haya kusisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za uendeshaji na uongozi mzuri wa taasisi ya fedha kama hii. Naomba kamwe nisieleweke kuwa nina mashaka na Menejimenti au Bodi iliyopo. Sina mashaka kabisa. Nina imani nao sana kwamba wana uwezo wa kutuvusha na kutupeleka kwenye neema. Nayasema haya kusisitiza umuhimu wake na kutaka yazingatiwe wakati wote.

Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jambo lingine muhimu sana kwa maendeleo ya benki hii ninalopenda kulisisitiza ni kuwa na sera ya mikopo iliyo nzuri. Aidha, hakikisheni kwamba mnakuwa makini katika ukopeshaji na ulipaji wa mikopo. Nimefahamishwa kuwa Benki hii ambayo ni maarufu kwa jina ”Benki Pekee Kwa Wote” itatoa mikopo kwa wanawake na wananchi wote kwa ujumla, wenye biashara kubwa, za kati na ndogondogo. Hii ni sahihi kabisa. Hata hivyo, ili benki hii iendelee kukua na kustawi na iwe na maendeleo endelevu na kutimiza malengo yake kama ilivyokusudiwa lazima mikopo itolewe kwa uangalifu na hakikisheni inalipwa kwa wakati. Vile vile, muwe na msimamo thabiti katika kuwabana na kuwawajibisha wasiolipa mikopo yao kwa mujibu wa masharti ya mikopo.

Natoa wito kwa wale watakaokopa katika Benki ya Wanawake waitumie vizuri na walipe mikopo yao kwa wakati ili waepukane na madhara yanayosababishwa na kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati stahiki. Kwa upande wa Benki lazima kuzingatia taratibu za kutoa mikopo kabla ya kutoa na kuhakikisha kuwa wakopaji wanafuatiliwa vizuri ili kupunguza hasara. Hii itaiwezesha benki kuwa na msingi imara ulio endelevu na kuweza kuwafikia wadau wake (wanawake) wengi mijini na vijijini kama lilivyo lengo la Benki hii. Narudia kusisitiza kuwa ni muhimu kwa wanawake kujijengea tabia na utaratibu wa kuweka akiba zao katika benki hii. Licha ya kuwahakikishia usalama, benki inatoa fursa nyingi za kiuchumi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri na viongozi wenzako Wizarani na katika UWT kufanya juhudi za makusudi za kutoa elimu kwa wanawake wote nchini. Katika kufanya hivyo muwaelimishe pia kuwa, huwa rahisi kwa benki kuwakopesha watu wenye akaunti na ambao hufanya shughuli zao za mapato na malipo kupitia benki hiyo.

Ni matarajio yangu na ya wanawake wote nchini kuwa huduma za Benki hii zitawafikia kwa urahisi. Hii ina maana ya Benki kuwa na matawi maeneo mengi nchini. Hili ni jambo la msingi ambalo Benki yetu hii haina budi ilipatie jibu sawia. Nimefurahi kusikia kwamba katika mpango mkakati wake, benki hii imejipanga kufanya hivyo siku za usoni. Naomba Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ishirikiane kwa karibu na Menejimenti ya Benki katika utekelezaji wa shabaha hii ya kufungua matawi katika mikoa hapa nchini. Naomba pia nitahadharishe kuwa, ufunguzi wa matawi katika mikoa ufanyike baada ya kuimarika kwa Benki. Jambo hili lisifanyike kwa nia ya kupendezesha wadau bila kujali uwezo wa Benki kumudu kufanya hivyo. Msipozingatia kanuni hiyo ya msingi benki itadhoofika baada ya muda si mrefu na uhai wake utakuwa hatarini. Angalieni mifano ya Benki nyingine nchini, hususan zile za kigeni ambazo zilichukuwa muda kabla ya kufungua matawi nje ya Dar es Salaam. Walifanya hivyo ili kujipa muda wa kukua na kujijenga. Msikubali kufanya kinyume chake.

Jitihada Nyingine za Kuwawezesha Wanawake

Mheshimiwa Waziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana

Ni muhimu nikaeleza pia kwamba, jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi hazianzi leo kwa uanzishaji wa hii Benki. Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kwa nia ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake na vijana. Kumekuwepo na mipango na programu kadhaa kwa lengo hilo. Kwa mfano, kuna Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (WDF), ambao umekuwa unatoa mikopo ya masharti nafuu kwa wanawake kupitia Halmashauri za Wilaya na Miji nchini. Wanawake zaidi ya 300,000, wamefaidika na mfuko huu na wengi zaidi watanufaika. Upo mfuko wa Rais wa Kujitegemea na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unaojulikana kama mabilioni ya JK, ulioanzishwa mwaka 2006 ambapo wanawake wengi wamenufaika. Serikali pia, imewezesha mashirika kadhaa yasiyokuwa ya Kiserikali kufanya kazi nchini na kunufaisha wanawake wengi. Tutaendelea kuongeza fedha katika mifuko hiyo na kurahisisha mazingira ya kazi kwa NGO’s zinazosaidia wanawake nchini. Pia tutaendelea kuongeza mtaji wa Benki hii mara kwa mara.

Aidha, wanawake wamewezeshwa kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya biashara ambapo wamewezeshwa kupata masoko ya bidhaa zao na kuwa kichocheo cha kuongeza bidhaa wanazozalisha. Wanawake, pia, wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa madhumuni ya kutumia vizuri mitaji pamoja na mikopo wanayopatiwa. Serikali katika awamu hii imetoa msukumo mkubwa wa wananchi kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa yaani SACCOS. Kwa ajili hiyo SACCOS nyingi zimeanzishwa nchini na kuwa chombo cha kifedha ambacho wanawake wengi wameweza kupata mikopo ya kufanya shughuli zao. Benki ya Wanawake tunayoizindua leo inaweza kuwanufaisha wanawake wengi zaidi kama itaweka mkakati mahususi wa kufanya kazi na SACCOS hapa nchini. Kufanya hivyo pia kutasaidia benki kusogeza huduma zake karibu na walipo wadau wake. Itasaidia kujijenga na kutanua huduma zake. CRDB ni mfano mzuri wa benki iliyotumia mfumo wa SACCOS kujijenga, kujitanua na kuwa karibu na watu.

Kilimo Kwanza

Ndugu Wananchi;

Kabla ya kumaliza hotuba yangu ningependa kutoa ombi maalum kwa uongozi na menejimenti ya Benki yetu hii mpya kuwa, katika kutengeneza sera ya mikopo wasisahau mikopo kwa sekta ya kilimo. Naelewa hisia na hasa hofu za mabenki kukopesha sekta ya kilimo. Nawaomba msizipuuzie hofu hizo hata kidogo ila msitishike mno wala kuendekeza hofu hizo na zikawafanya muinyanyapae sekta ya kilimo. Zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo kwa maisha yao na kwa maendeleo yao. Na, wengi wa hao ni wanawake. Hivyo mkitoa mikopo kwa sekta ya kilimo mtawanufaisha wadau wenu wengi na kuwafurahisha. Jambo muhimu ambalo hamna budi kulizingatia ni kuwa makini kwa upande wa mtu na shughuli mnayoitolea mkopo. Nawaomba mchague sekta ndogo au shughuli za kilimo ambazo hatari za kupata hasara si kubwa, mtoe mikopo kwa kina mama wanaojihusisha nazo. Mkifanya hivyo, pia mtakuwa mmechangia katika utekelezaji wa mkakati mpya wa kusukuma kilimo kwa kasi mpya, maarufu kwa Kilimo Kwanza.

Namalizia kwa kuwapongeza tena wanawake wote nchini kwa mafanikio makubwa waliyopata ya kuweza kuwa na benki yao. Nawaomba mdumishe na kuendeleza umoja na mshikamano wenu ili kuhakikisha kuwa benki yenu hii muimiliki na kuiendesha vizuri kwa maslahi ya wanawake na maendeleo yao. Baada ya kusema hayo, natamka kuwa Benki ya Wanawake Tanzania imezinduliwa rasmi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Mungu Wabariki Wanawake Wote Nchini.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA