highlights


Reports and Policies

News and Events

Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kuadhimishwa Mkoani Shinyanga

Tanzania inaungana na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike inayofanyika tarehe 11 Oktoba kila mwaka ikiwa ni mwitikio wa Azimio la Umoja huo lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 2011.

Akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam Mrugenzi wa Idara ya Watoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jammii, Wazee Jinsia na Watoto Bi. Magareth S. Mussai amesema azimio hili linazitaka nchi wanachama kuadhimisha siku hii kwa ajili ya kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukatili mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni.

Aliongeza kuwa lengo kuu la Umoja wa Mataifa kwa kutenga siku hii ni kutafakari uzingatiaji wa haki za Mtoto wa Kike; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha upatikanaji wa haki hizo ndio maana mwaka huu Maadhimisho haya yatafanyika kitaifa katika mkoa wa shinyanga tarehe 11 Oktoba na yamelenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutetea haki za watoto wa kike na kutoa fursa ya kutathimini changamoto zinazowakabili watoto hapa nchini.

Aidha Mkurugenzi wa Idara ya Watoto ameitaja Kauli Mbiu ya Maadhimisho haya kuwa ni ‘’Mimba na Ndoa za Utotoni Zinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto wa Kike.” Akisisitiza kuwa Kaulimbiu hii inatukumbusha wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto hawaolewi katika umri mdogo kwa kuwa kufanya hivi kunawanyima haki yao ya msingi ya kuendelea na masomo na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao za kupata elimu kwa manufaa yao, familia na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo wasichana wapatao milioni moja wanatarajiwa kuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18 duniani kote.

Aliongeza kuwa katika Bara la Afrika, asilimia 42 ya wasichana wote huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 huku akiongeza kuwa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa mkoa unaoongoza kwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni ni Shinyanga ambayo ina asilimia 59 ndio maana maadhimisho yanafanyiko mkoani humo ili kutafakari kwa kina namna bora ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema kiwango cha ndoa za utotoni hapa nchini kipo kwa kiasi kikubwa kwa wasichana wenye elimu ndogo, wasichana wanaotoka katika familia maskini na wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini.