highlights


Reports and Policies

News and Events

WaziriSophia Simba katika mkutano 54 wa wanawake New York

Waziri Wa Nchi Ofisi Ya Rais Utawala Bora Mhe. Sophia Simba Akishiriki Na Kuongoza Ujumbe Wa Tanzania Katika Mkutano Wa 54 Wa Kamisheni Ya Umoja Wa Mataifa Kuhusu Hali Ya Wanawake.

Tanzania imesisitiza umuhimu wa wanawake wanaoishi katika maeneo yenye migogoro na vita kushikiriki katika mchakato wa majadiliano ya kutafuta amani.

image
PICHA NA HABARI KWA HISANI YA UBALOZI WA TANZANIA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. Sophia Simba ameyasema hayo wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya tathimini ya utekelezaji wa tamko la mkutano wa nne wa Beijing. Pamoja na matokeo ya mkutano maalum wa 23 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama.

Waziri Simba anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa huo 54 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Wajumbe hao ni kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Amesema wanawake ni lazima washiriki katika mikutano ya kutafuta amani kwa sababu ndio waathirika wakubwa itokeapo vita na mapigano.

Anasema Simba ni vema tukajikumbusha kwamba wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa yanapotokea mapigano ya kutumia silaha. Kwa sababu hiyo wanatakiwa kuwa sehemu ya majadiliano ya kutafuta amani.

Aidha akasema kuwa Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia upatikanaji wa amani na usalama sehemu mbalimbali hususani eneo la Maziwa Makuu. Inaihimiza jumuia ya kimataifa kutekeleza kwa vitendo matamko mbalimbali ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama.

Akizungumzia namna serikali za Tanzania Bara na Visiwani zinavyozingatia kwa vitendo usawa wa jinsia na uwezeshwaji wa wanawake.

Waziri amewaeleza wajumbe wa mkutano huo, kwamba viongozi wa serikali zote mbili wameonyesha utashi wa kisiasa kuhusu masuala yanayohusu haki za wanawake.

Akasema Rais Jakaya Kikwete na viongozi wote katika nafasi zao mbalimbali wanaonyesha utashi mkubwa wa kisiasa katika kutetea hali bora ya mwanamke kiasi kwamba hivi sasa nchini Tanzania usawa na jinsia na uwezeshaji si suala ya mjadala tena.

Kwa upande wa Tanzania, suala la usawa wa jinsia na uwezeshwaji wa wanawake si jambo la majadiliano tene, huko tumeshatoka, kilichopo sasa ni utekelezaji wa mipango ya kufanikisha usawa huo na uwezeshaji; anasisitiza Simba.

Anaongeza kuwa kutokana utashi wa kisiasa unaonyeshwa na viongozi, kumekuwapo na mafanikio makubwa yakiwamo ya kuingizwa kwenye katiba zote mbili nafasi za wanawake katika vyombo vya kutunga sheria na kutoka maamuzi yaani Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Aidha akaongeza kuwa masuala ya jinsia pia yameainishwa katika utekelezaji wa programu za kukuza uchumi na kupinguza umaskini maarufu kama MKUKUTA na MKUZA.

Akasema mafanikio makubwa pia yamepatikana kwa upande wa elimu ya mtoto wa kike.Idadi ya watoto wa kike kuanzia shule za msingi , sekondari na elimu ya juu imeongezeka kwa kiwango kikibwa. Na serikali inaamini kwamba kumpatia elimu mtoto wa kike sit u kwamba ni mtaji kwa taifa lakini pia kunasaidia sana kupunguza ndoa za umri mdogo.

Changamoto kubwa inayotukabili kwa sasa kwa upande wa elimu ya mtoto wa kike ni namna ya kuboresha mazingira anayosomea ili kumfanya aendelee kubaki shuleni na kufanya vizuri kimasomo anabainisha Waziri Simba.

Kuhusu uwezeshwaji, anasema serikali zimeweka mazingira bora yanayomwezesha mwanamke kupata mitaji ya biashara, elimu ya biashara na pia serikali imeanzisha bank ya wanawake.

Pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, Tanzania imeungana na nchi nyingine katika kukiri kwamba miaka kumi natano baada ya Tamko la kihistoria la Beijing, bado utekelezaji wa tamko hilo unakabiliwa na changamoto mbalimbali

Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mila na tamaduni zinazomkandamiza mwanamke, ukosefu wa rasilimali za kumwendeleza mwanamke, ukosefu wa takwimu sahihi kuhusu hali ya mwanamke mwanamke anakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Akasema serikali za Tanzania zipo tayari kushirikiana na kufanya kazi na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi zisizo za kiserikali katika kufanikisha upatikanaji wa fursa na haki sawa kwa maendeleo ya mwanamke.