Reports and Policies

Siku ya Haki ya Mtoto Tarehe 20 November 2016

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa taarifa kuwa; Tanzania itaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Haki ya Mtoto itakayoadhimishwa Duniani kote tarehe 20 Novemba, 2016. Chimbuko la maadhimisho haya ni kipengele cha 9 cha Azimio na 836 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Desemba 14, 1954 lililopendekeza Nchi zote Wanachama kuadhimisha siku hiyo.

Mwaka 1959, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 20 Novemba ya kila mwaka kuwa ni siku ya Haki za Mtoto Duniani, kufuatia kupitishwa kwa siku ya Haki ya Mtoto na Baraza hilo, mwaka 1989 Baraza kwa kauli moja lilipitisha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto na kuanzia kipindi hicho siku hiyo ikatambuliwa kuwa “Siku ya Haki ya Mtoto’

Lengo la kuwapo kwa siku hii ni kudumisha undugu, maadili, kufahamiana na kujenga mshikamano miongoni mwa watoto katika jamii zote duniani. Tanzania tumekuwa tukiadhimisha siku hii kila mwaka kwa watoto kuendesha midahalo ya kujadili utekelezaji wa haki za mtoto, kufanya maandamano na kucheza michezo mbalimbali.

Katika matukio haya watoto hupata fursa ya kujua kwa undani jinsi Serikali na wadau walivyofanya juhudi mbalimbali katika utekelezaji wa haki za watoto nchini. Vilevile watoto hutumia fursa hii kutoa ushauri kwa serikali ya jinsi ya kuboresha ufanisi wa afua zinazochangia kutoa huduma za haki ya mtoto.

Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtoto Duniani yanatoa fursa kwa Serikali, wazazi, walezi, wadau na jamii kwa ujumla katika ngazi mbalimbali kutafakari utoaji wa Haki za Mtoto katika kipindi cha mwaka mmoja. Haki kuu za mtoto ni Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na Kutobaguliwa.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu- TAMISEMI inatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kushirikiana na wadau wa maendeleo walioko katika maeneo yao kuadhimisha siku hii muhimu kwa kadri watakavyoona inafaa, ili kuongeza uelewa wa haki za mtoto kwa watoto wenyewe, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.

Kupitia maadhimisho haya, Wizara inapenda kutumia fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote wa kidato cha nne wanaomaliza mitihani na kuanza maisha mapya. Aidha, Wizara inawakumbusha kwamba kuhitimu kidato cha nne ni mwanzo wa safari ndefu ya kielimu katika kufikia ndoto na matarajio waliyonayo kuwa raia wema na wenye mchango na tija kwa taifa.

Mwisho, wazazi na walezi wenye watoto wa kike wanasisitizwa wasiwaowaozeshe bali watoto hao. Serikali haitasita kuchukuwa hatua stahiki kwa mzazi/mlezi au mtu yeyote atakayehusika na kumuoza au kumuoa mtoto anayetakiwa kuendelea na masomo.

Imetolewa na

Ofisi ya Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
15/11/2016