MCDGC Publication

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 15 – 19 Oktoba 2011 ni siku maalumu za kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Siku hizi zitatumiwa na Wizara kujenga uelewa wa pamoja kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii yetu. Hii ni pamoja na kukumbushana tulikotoka, tulipo na tunapoelekea katika muktadha wa Maendeleo ya Jamii, jinsia, watoto na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali tangu tulipopata uhuru tarehe 9 Desemba, 1961 hadi kipindi hiki muhimu ambapo tunasheherekea miaka 50 ya Uhuru.

Tarehe 15 Oktoba, 2011 Wizara itaanza kutangaza mafanikio yake kupitia vyombo vya Habari. Siku ya Jumatatu tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2011 Wizara itaendelea na matangazo ikiwa ni pamoja na kufungua maonesho siku tatu (3) katika viwanja vya Mnazi mmoja.

Vilevile kutakuwa na kongamano la Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikisha wakongwe wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Jamii. Katika viwanja vya maonesho wananchi watapa maelezo mbalimbali kuhusu dhana ya maendeleo ya jamii, Vyuo vya Wizara, Maendeleo ya jinsia na Wanawake, Hali ya Watoto na ustawi wao, Uratibu na Usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ufafanuzi wa sera za Wizara, na sheria ya NGOs Na. 24 (2002) na sheria ya Mtoto Na. 21 (2009).

Wananchi wote wa mkoa wa Dar es salaam na maeneo ya jirani mnakaribishwa kuhudhuria maonesho ya Wizara ili kupata maelezo kuhusu mafanikio yaliyofikiwa katika masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, watoto na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali tangu Tanzania Bara ilipopata uhuru wake mwaka 1961. Hivyo kwa hakika ninasema kuwa, kwa pamoja tumethubutu, tumeweza, tunazidi kusonga mbele.