MCDGC Publication

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA FAMILIA DUNIANI

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA FAMILIA TAREHE 15/05/2017

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatoa taarifa kuwa, tarehe 15 Mei, itakuwa siku ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia. Maadhimisho haya, yanatokana na Tamko la Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 47/237 lililopitishwa tarehe 20 Septemba, 1993 likizitaka nchi wanachama kuadhimisha siku hii katika kuenzi familia kama kitovu cha maendeleo katika jamii.

Kwa mwaka 2017, Maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya Mkoa, ambapo mkoa utapanga utaratibu na shughuli zitakazofanyika wakati wa maadhimisho kwa kuzingatia mazingira ya eneo husika; na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walioko katika mikoa yetu.

Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka 2017 Kaulimbiu ni “Elimu na Malezi Bora kwa Ustawi wa Familia”. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali, Asasi Za Kiraia, Taasisi za dini, sekta binafsi, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutafakari na kuwekeza zaidi katika haki ya elimu ya watoto kwa kuwarithisha maarifa yatakayowapa mbinu na weledi wa kutoa mchango thabiti katika kufikia maendeleo endelevu ya taifa letu.

Katika kuadhimisha siku hii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalinu (Mb), ataongea na vyombo vya habari katika Mkutano utakaofanyika ukumbi wa Waandishi wa habari, Eneo la Ofisi ya Bunge mjini Dodoma tarehe 15 Mei, 2017, saa 5.00 Asubuhi.
Wizara inatoa wito, kwa Mamlaka za Mikoa kuwafahamisha wananchi na kuwashirikisha katika kuadhimisha siku hii adhimu, ili kutoa fursa ya kutafakari na kuwa na uelewa wa pamoja katika kuitikia kaulimbiu ya mwaka huu 2017.

Kwa namna ya pekee, napenda kutoa wito kwa vyombo vya habari kushirikiana na Wizara, Mikoa na wadau wengine katika kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia ikiwa ni pamoja na kuitikia utekelezaji wa kaulimbiu ili kuhakikisha kuwa tunaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha tunaendelea kuwa na Taifa lenye watoto walio na elimu, maadili mema na nidhamu katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.


Imetolewa na,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto
12/5/2017