MCDGC Publication

Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto

Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kutekeleza azma yake ya kujenga jamii ya watu wenye afya, wanaoheshimu kazi na haki kwa kuzingatia usawa wa jinsia, kwa kutoa mafunzo mbalimbali katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Vyuo Maendeleo ya Jamii nchini kote.

Jukumu kubwa la Sekta ya Maendeleo ya Jamii ni kuwaandaa watu kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Sera, Progamu na Mipango ya Sekta zote zinazohusika na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Ili kufanikisha hilo, yafuatayo yametekelezwa;

- Serikali imeanza kutekeleza mapendekezo ya kuboresha mazingira ya Wataalamu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii ikiwa ni pamoja na kuwapatia watumishi wa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ruzuku ya sh. 3,600,000/= kwa mwaka 2008/2009 na sh. 7,200,000 /= kwa mwaka 2009/2010.
- Idadi ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii imeongezeka kutoka vinne (4) mwaka 2005 hadi kufikia vyuo tisa (9) mwaka 2008.
- Wizara imeanzisha kozí ya Shahada katika Chuo cha Tengeru na Stashahada katika Vyuo (4) vya Rungemba, Missungwi, Buhare na Monduli na Vyuo 4 vya Mabughai, Mlale, Ruaha na Uyole ambavyo vilikuwa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vimebadilishwa na kuwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na vitatoa cheti cha msingi na cheti.
- Idadi ya udahili wa wanachuo katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii imeongezeka kutoka 423 mwaka 2006/07 hadi kufikia 736 mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 73.9
- Mwaka 2006 hadi 2008 jumla ya watumishi 438 wa Halmashauri na Kata wamepatiwa mafunzo mbalimbali kuhusu: usimamizi, matumizi ya mbinu shirikishi, kuandaa andiko la miradi, ujasiriamali, kuingiza masuala ya jinsia katika mipango, haki za watoto, usimamizi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
- Mwaka 2005/2006 Halmashauri za Morogoro, Rombo, Handeni, Muheza, Iringa, Rufiji, Songea, Singida, Shinyanga na Tabora zilipatiwa pikipiki moja kwa kila Halmashauri ili kuwawezesha wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuwafikia wananchi kwa urahisi.
- Wizara imefanya ukarabati wa miundo mbinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, ambapo Vyuo 34 vimefanyiwa ukarabati wa majengo na miundo mbinu. Vyuo hivyo ni Bigwa, Buhangija, Chala, Chilala, Chisalu, Gera, Handeni, Ifakara, Ikwiriri, Karumo, Kilosa, Kilwa masoko, Kisarawe, Kiwanda, Kisangwa, Malampaka, Malya, Mamutukuna, Masasi, Mbinga, Muhukuru, Munguri, Msaginya, Msinga, Msingi, Musoma, Mtawanya, Nzovwe, Nzega, Rubondo, Same, Sofi, Ulembwe, Urambo.
- Maboresho ya vyuo yamechangia katika kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaopatiwa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi ndani na nje ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kutoka 25,531 mwaka 2005/06 hadi 29,557 mwaka 2008/09.
- Mwezi Desemba 2008 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliziagiza Halmashauri zote nchini kuajiri Wataalam wa Maendeleo ya Jamii katika ngazi za Kata na kuwaendeleza kitaaluma wale waliokwisha ajiriwa.

2. Kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mafunzo yanayotolewa katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi: Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi vinawapatia wananchi stadi mbalimbali za maisha zinazowawezesha kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kuchangia katika vita dhidi ya umaskini. Katika jitihada za kuviwezesha vyuo kufanikisha azma hiyo, wizara imetekeleza yafuatayo;

- Mwaka 2006/07 Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya Chala, Msaginya, Ulembwe, Kiwanda, Tango, Chilala, Muhukuru, Nandembo, Mtawanya, Ifakara, Kilosa, Malampaka, Bariadi, Kihinga, Sikonge, Malya, Gera, Karumo, Msingi na Chisalu vilipatiwa pikipiki 20 (moja kwa kila chuo) ili kupunguza tatizo la usafiri na kufanikisha mafunzo nje ya vyuo.
- Jumla ya wananchi 11,4488 waliopata mafunzo katika vyuo vya maendeleo ya wananchi mwaka 2006 – 2009 kati yao wanawake walikuwa 52,672 na wanaume 61,8

3. Uingizwaji wa masuala ya jinsia katika Sera, Mipango na Mikakati mbalimbali: Uingizwaji wa masuala ya jinsia katika uandaaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanachangia katika kuleta maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla. Katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na usawa wa kijinsia wizara imetekeleza yafuatayo:

- Wizara Kwa kushirikiana na wadau imeanzisha Dawati la Jinsia katika ngazi ya Halmashauri, Mkoa, Wizara na Idara zinanzojitegemea kwa ajili ya kufuatilia uingizwaji wa masuala ya Jinsia katika Sera, Mikakati, Programu, na Mipango mbalimbali katika ngazi husika.
- Wizara ilitoa mafunzo kuhusu uingizaji wa masuala ya jinsia katika Sera, Mikakati, Mipango na bajeti kwa washiriki 473 wa kada mbalimbali.

4. Kuwawezesha wanawake kiuchumi :

5. Katika kuhakikisha kuwa Wanawake wanachangia pato la Taifa kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali Wizara imefanikisha kutekeleza yafuatayo:
- Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake(WDF), Wizara imeendelea kutoa mikopo kwa wanawake kupitia Halmashauri zao. Kati ya mwaka 2006 hadi 2009, jumla ya Halmashauri 88 zimepatiwa mikopo ya kiasi cha Shilingi 708,000,000 ambapo Halmashauri 44 zimerejesha kiasi cha shilingi 252,461,274.
- Wizara kwa kushirikiana na wadau imekamilisha uanzishwaji wa Benki ya Wanawake Tanzania ambayo imeanza kutoa huduma zake tarehe 28/07/2009. Tawi la kwanza liko katika jengo la Posta ya Zamani upande wa Mtaa wa Mkwepu Dar-es-Salaam. Lengo la Benki hii ni kutoa huduma imara za kibenki na mafunzo ya ujasiriamali hususan kwa wanawake.
- Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009 Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake 170 wanaoishi na virusi vya UKIMWI kutoka mikoa ya Dar-es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Pwani, Tanga na Arusha.
- Katika kipindi cha 2006- 2009 Wizara ilitoa mafunzo kwa wasichana waliozaa katika umri mdogo na yatima wapato 237, katika Vyuo vya Ilula, Kiwanda, Mamtukuna, Nzovwe, Tarime, Ulembwe na Uyole. Wasichana hao walishiriki katika mafunzo hayo pamoja na watoto wao. Mafunzo waliyopatiwa yalihusu malezi ya watoto na ujasiriamali.

6. Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na albino

Serikali inaendelea na juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia hususan wanawake, watoto na albino uliokithiri hapa nchini. Katika kufanikisha azma hii Wizara imetekeleza yafuatayo:

- Mwaka 2006 Wizara ilidurusu Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto na kuuongezea muda wa utekelezaji kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2015. Mpango huo unalenga katika kubadilisha sheria zinazowakandamiza wanawake na watoto, kutoa elimu, mafunzo na uhamasishaji kwa wananchi kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na albino, kutoa huduma zinazofaa kwa waliotendewa ukatili na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya mila na desturi zinazoendeleza ukatili.
- Wizara Ilitoa mafunzo kuhusu utokomezaji wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa watumishi wa Serikali 190 wanaosimamia utekelezaji wa sheria wakiwemo Polisi, Askari Magereza na Mahakimu. Aidha, wanawake 200 walipatiwa mafunzo ya uelewa wa haki zao na masuala ya jinsia.
- Wizara iliratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji hapa nchini. Aidha, iliandaa mkutano uliowahusisha washiriki 34, wakiwemo Makamanda wa Polisi wa Wilaya, Mahakimu wa Wilaya, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri na Wawakilishi kutoka Sekretariati za Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha unaohusu ukeketaji.
- Wizara kwa kushirikiana na taasisi zinazopambana na ukeketaji wanawake iliendesha semina kwa Waheshimiwa Wabunge 25 kutoka Mikoa 14 yenye mila za ukeketaji wa wanawake kwa lengo la kuweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hili.
- Wiizara iliratibu uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya Kataa Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto uliofanywa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24, Mei 2008. Kampeni hii inaendelea nchini kote kwa kusaini vikonyo kupitia mtandao wa Vodacom na mbio za Mwenge wa Uhuru zenye kaulimbiu inayosomeka Pinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake, Watoto na Albino.

7. Kuongeza ushiriki wa Wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi wa Kisiasa, Kiutendaji na nafasi za Maamuzi kufikia asilimia 50 ifikapo 2010

- Wizara imeandaa Rasimu ya Mkakati wa Kuwezesha Tanzania Kuongeza Ushiriki wa Wanawake Katika Ngazi Mbalaimbali za Uongozi wa Kisiasa, Kiutendaji na Nafasi za Maamuzi, ili kuhakikisha kuwa uwakilishi wa asilimia 50 unafikiwa.
- Mwaka 1995 baada ya kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viti maalumu vilitakiwa kuwa asilimia 15 ya viti vyote. Idadi hiyo iliongezeka kufikia asilimia 20 mwaka 2000 na asilimia 30.4 mwaka 2005.
- Ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi ya kisiasa na kiutendaji umeongezeka, kwa mfano Idadi ya Mawaziri imeongezeka kutoka asilimia 15, mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2009
- Iidadi ya Wabunge imeongezeka kutoka wabunge 63, mwaka 2004 hadi 93 mwaka 2009, idadi ya Wabunge waliochaguliwa kwenye majimbo imeingezeka kutoka 12 hadi 17, na Naibu Spika wa Bunge ni Mwanamke.
- Idadi ya Makatibu Wakuu imeongezeka kwa asilimia 30.2 kati ya mwaka 2004 hadi 2009.
- Idadi ya makamishina wanawake imeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2004 hadi asilimia 54 mwaka 2009.
- Idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufaa wameongezeka kutoka asilimia 11, (2004) hadi asilimia 25 mwaka 2009
- Mahakama Kuu ya Tanzania idadi ya Majaji imeongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2004 hadi asilimia 27, mwaka 2009.

8. Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu Wanawake na Watoto

Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009, Wizara imeandaa na kuwasilisha taarifa zifuatazo:-

- Mwaka 2006 Wizara iliwasilisha Taarifa ya Nne na ya Tano zinazohusu utekelezaji wa CEDAW.
- Serikali iliandaa Taarifa ya Sita ya Mkataba huo na kuiwasilisha mwezi Januari, 2008. Wizara ilizitetea taarifa hizo tatu kwa pamoja mwezi Julai, 2008.
- Taarifa ya Awali ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto katika Umoja wa Afrika mwezi Januari , 2007 na Taarifa za utekelezaji wa Itifaki za Nyongeza za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto kuhusu Ushirikishaji wa Watoto katika Migogoro ya Kivita, Uuzaji wa Watoto, Uhusishaji wa Watoto katika Vitendo vya Ukahaba, na Upigaji picha za Udhalilishaji wa Watoto. Serikali ilizitetea Itifaki hizo mbili katika kikao cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika Geneva, Uswis tarehe 29 Septemba, 2008.
- Katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa wizara ilitekeleza yafuatayo:
- Ilishiriki katika vikao mbalimbali vya kikanda na kimataifa ambavyo ni Kikao cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake Duniani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto, mikutano ya Nchi za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Nchi za Maziwa Makuu, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
- Wizara imeratibu shughuli za Baraza la Watoto la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lenye wajumbe 54 kutoka Tanzania Bara na Visiwani kwa kuhakikisha kuwa linafanya vikao vyake mara mbili kila mwaka.
- Mabaraza ya watoto yameanzishwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na katika wilaya 17. Uanzishwaji wa mabaraza haya ni utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto pamoja na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za Mtoto.
- Kuandaa Mkutano wa Nchi 12 za Kusini na Mashariki mwa Afrika kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto. Mkutano huo uliofanyika Arusha tarehe 18 – 21 Februari 2008. Mojawapo ya Maazimio ya Mkutano huo ni kila nchi kuandaa Sera ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
- Rasimu ya Sera hiyo imeandaliwa ili kutoa mwongozo kwa wadau wanaotekeleza na kutoa huduma kwa watoto wa umri wa miaka 0-8 kwa ajili ya kuboresha maisha yao.
- Mafunzo yalitolewa kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 24 na Maafisa Maendeleo ya Jamii 120 kwenye Secretariati za Mikoa na Halmashauri kuhusu haki zinazohusu uhai, ulinzi, maendeleo, ushiriki na kutobaguliwa kwa watoto.
- Wizra imeandaa Rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Familia inayotoa mwelekeo wa jinsi ya kubaini vikwazo vya kimaendeleo ndani ya familia na namna ya kukabiliana navyo. Rasimu ya Sera hiyo imesilishwa katika ngazi za maamuzi ili iweze kupitishwa kwa utekelezaji.
- Wizara imetayarisha Kitini cha Jamii kuhusu Elimu ya Idadi ya Watu na Maisha ya Familia (Population and Family Life Education). Kitini hiki kimelenga kuboresha maisha ya familia kwa njia ya kuwaelimisha kuhusu mazingira, UKIMWI, lishe, elimu ya uzazi, na Jinsia.
- Wizara imeratibu maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, Siku ya Mtoto wa Afrika, na Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambazo zinaadhimishwa kitaiafa na kimataifa kila mwaka.

9. Usimamizi na uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali
- Wizara imewezesha uundwaji na uzinduzi wa Bodi ya Taifa ya Uratibu wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali mnamo tarehe 10 Desemba, 2007. Hadi sasa Bodi hiyo imefanya vikao 16 vya kuratibu sekta ya NGOs katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tanga, Arusha na Dar-es Salaam. Kufanyika kwa vikao hivi katika mikoa hiyo kumeongeza ushirikiano kati ya Sekta ya NGOs, wananchi na Serikali.
- Wizara imeanzisha Tovuti inayotumika kupata taarifa kuhusu utendaji wa sekta ya NGOs. Tovuti hii imetoa fursa kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu utendaji wa NGOs ili kuongeza uwazi na uwajibikaji na kupunguza ubabaishaji kwa baadhi ya NGOs ambazo hazina uaminifu katika utendaji wa kazi zao.
- Wizara imesajili Mashirika 3,263, kati ya haya 2,588 ni usajili na 675 yamepatiwa cheti cha ukubalifu chini ya Sheria ya NGOs Namba 24 ya 2002 kama inavyooneshwa kwenye jedwali Na. 8. Aidha, Mashirika haya yanatakiwa kutoa taarifa ya kazi ya mwaka na taarifa ya fedha ili kupima mafanikio ya malengo yao.
- Wizara imetoa mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii 150 katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara. Mafunzo hayo yaliwaongezea uelewa kuhusu taratibu za usajili wa NGOs, Sera ya Taifa ya NGOs, Sheria ya NGOs Namba 24 ya mwaka 2002, ufuatiliaji, tathmini na uchambuzi wa taarifa za NGOs. Aidha, mafunzo hayo yalilenga katika kukuza na kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya NGOs na Halmashauri kwa kuanzisha mchakato wa kuwateua Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa Wasajili Wasaidizi wa NGOs.
- Wizara imeanzisha Benki ya Takwimu za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwapatia wananchi fursa ya kupata taarifa za NGOs yoyote kuhusu utendaji kazi wake. Utaratibu huu umesaidia sana wananchi kubaini baadhi ya NGOs ambazo hazitekelezi malengo yao kwenye maeneo ya kazi.
- Wizara imewezesha kukamilisha Mikataba kati ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 25 ya kimataifa. Mikataba hii imesaidia kuainisha majukumu ya NGOs na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya NGOs ili kukuza uwazi na uwajibikaji.