MCDGC Publication

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO ILIYOTOLEWA NA MKURUGENZI WA WATOTO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE ILIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA IDARA YA HABARI/MAELEZO, DAR ES SALAAM TAREHE 5/10/2016

Ndugu Wanahabari,
Tanzania inaungana na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike inayofanyika tarehe 11 Oktoba kila mwaka ikiwa ni mwitikio wa Azimio la Umoja huo lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 2011. Azimoi hili linazitaka nchi wanachama kuadhimisha siku hii kwa ajili ya kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukatili mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni.

Aidha, Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa lengo la kutafakari uzingatiaji wa haki za Mtoto wa Kike; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha upatikanaji wa haki hizo.

Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yatafanyika kitaifa mkoa wa shinyanga tarehe 11 Oktoba na yamelenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutetea haki za watoto wa kike na kutoa fursa ya kutathimini changamoto zinazowakabili watoto hapa nchini.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ni ‘’Mimba na Ndoa za Utotoni Zinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto wa Kike.” Kaulimbiu hii inatukumbusha wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto hawaolewi katika umri mdogo kwa kuwa kufanya hivi kunawanyima haki yao ya msingi ya kuendelea na masomo na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao za kupata elimu kwa manufaa yao, familia na Taifa kwa ujumla.

Ndugu Wanahabari,
Serikali na wadau wa haki za watoto tunaamini kuwa msichana mwenye umri chini ya miaka 18 anakuwa hajakomaa kimwili, kimaumbile na kisaikolojia ili aweze kumudu majukumu ya kifamilia na uzazi. Pia katika umri huu mtoto wa kike anatakiwa kuendelea kupatiwa elimu na stadi za maisha.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo wasichana wapatao milioni moja wanatarajiwa kuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18 duniani kote. Katika Bara la Afrika, asilimia 42 ya wasichana wote huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka18. Aidha takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa mkoa unaoongoza kwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni ni Shinyanga ambayo ina asilimia 59.

Mikoa mingine ni tabora 58%, Mara 55%, Dodoma 51%, Lindi 48%, Mbeya 45%, Morogoro 42%, Singida 42%, Rukwa 40%, Ruvuma 39%, Mwanza 37%, Kagera 36%, Mtwara 35%, Manyara 34%, Pwani 33%, Tanga 29%, Arusha 27%, Kilimanjaro 27%, Kigoma 29%, Dar es salaam 19%, na Iringa asilimia nane. Changamoto hii ni moja ya sababu ya Serikali na wadau kupeleka Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Kitaifa kufanyika katika Mkoa wa Shinyanga.


Ndugu Wanahabari,
Kiwango cha ndoa za utotoni hapa nchini kipo kwa kiasi kikubwa kwa wasichana wenye elimu ndogo, wasichana wanaotoka katika familia maskini na wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Aidha, Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 61 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 - 24 ambao hawakusoma na asilimia 39 ya wanawake wenye umri kati ya miaka hiyo wenye elimu ya msingi tu waliolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18 ukilinganisha na wanawake wenye umri kama huo ambao wana elimu ya sekondari au zaidi. Hali hii inafanya ndoa za utotoni kuwa ni sehemu ya unyanyasaji wa watoto wa kike.
Baadhi ya wasichana wanaotoka katika familia zenye umaskini uliokithiri wamekuwa wakikumbwa na tatizo la mimba na ndoa za utotoni. Ukosefu wa kipato katika familia hupelekea wazazi kutafuta namna yoyote ya kupata kipato kitakachowawezesha kukidhi mahitaji ya msingi ikiwa ni pamoja na kuozesha mtoto katika umri mdogo.

Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali inaendelea kuwaelimisha wazazi na walezi kutambua kwamba athari zinazotokana na uwepo wa ndoa za utotoni ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili. Hivyo kipindi hiki cha maadhimisho, kitatumika kuelimisha wazazi/walezi na jamii kutambua kwamba kumuozesha mtoto katika umri chini ya miaka 18 anakuwa muaathirika mkubwa wa ukatili wa kimwili na kingono.
Hivyo tunatoa wito kwa wazazi/walezi na jamii kuhakikisha wanaunga mkoni jitihada za serikali katika kuwapatia watoto haki ya kusoma, kuishi na kuwalinda dhidi ya ndoa za utotoni. Kila mtu awajibike kuhakikisha mtoto wa kike haolewi katika umri mdogo.

‘’Mimba na Ndoa za Utotoni Zinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto wa Kike.”

”AHSANTENI SANA”