MCDGC Publication

Taarifa Ya Mafunzo Ya Watendaji Wa Dawati La Jinsia, Morogoro

Taarifa Ya Mafunzo Ya Watendaji Wa Dawati La Jinsia Iliyofanyika Katika Ukumbi Wa Chuo Cha Tanesco Morogoro Tarehe 15 -17 Oktoba 2003

Mafunzo ya Watendaji wa Madawati ya Jinsia ni matokeo ya tathmini iliyofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuhusu uundaji wa Vitengo vya Jinsia katika Wizara. Tathmini hiyo ilifuatiwa na Warsha ya Wadau iliyopendekeza muundo wa madawati hayo uwe wa namna gani.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliyachambua maoni ya wadau na kuyafanyia kazi. Pamoja na mambo mengine wizara iliwasilisha katika Menejimenti ya Utumishi wa Umma ombi la kuunda Dawati la Jinsia katika wizara, idara, taasisi zinazojitegemea, mikoa na wilaya. Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitoa kibali cha kuingiza Dawati la Jinsia katika muundo wa wizara na idara/taasisi zinazojitegemea. Kibali hicho kilielekeza kuwa Dawati hilo liundwe na kuratibiwa katika Idara ya Mipango na pale ambapo Idara hiyo haipo, basi iwe Idara ya Utawala.