MCDGC Publication

TAMKO LA SERIKALI KUPITIA WIZARA YA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

TAMKO LA SERIKALI KUPITIA WIZARA YA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KULAANI KITENDO CHA UKATILI ALICHOFANYIWA MWANAFUNZI SEBASTIANI CHINGUKA MKOANI MBEYA
Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizosambaa kupitia picha ya video ikionyesha tukio lilitokea tarehe 28 September, 2016 saa 6 mchana la kikundi cha watu 4 walimu ambao walikuwa katika mafunzo ya ualimu kwa vitendo (mazoezi) shule ya sekondari ya kutwa, Mbeya (Mbeya Day) wakimshambulia mwanafunzi mmoja kwa viboko na ngumi kitendo kilichoashiria kuvuka mipaka ya utoaji wa adhabu kwa watoto shuleni na ukiukwaji wa Haki ya msingi ya Ulinzi kwa mtoto.
Mwanafunzi aliyefanyiwa ukatili huo anaitwa Sebastiani Chinguka anasoma kidato cha tatu (3) katika shule ya sekondari iliyotajwa hapo juu baada ya walimu hao ambao wako katika mafunzo ya ualimu kwa vitendo (mazoezi) kubaini kuwa mwanafunzi Sebastian hakufanya zoezi la somo la kiingereza kama wenzake ambao walimaliza kazi waliyopewa na mwalimu mmojawao.Aidha walimu hao hawakutaka kusikiliza maelezo ya mtoto ambayo yalikuwa na mashiko kutokana na ajali aliyokuwa ameipata mtoto huyo na hivyo kushindwa kutekeleza adhabu iliyotolewa na mwalimu sababu ya mauivu aliyokuwa nayo mguuni.
Shambulio hilo la kikatili ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ya uvunjifu wa haki za mtoto katika maeneo mbalimbali nchini.
Hii ni kinyume na Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, Mkataba ya Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika kuhusu haki na ustawi wa mtoto (1991) ambapo kwa pamoja inahimiza utowaji wa haki ya Kuishi,Kulindwa,Kuendelezwa,Kushiriki na Kutobaguliwa kwa watoto wote.
Pia katika Sehemu ya Pili ya Sheria ya Mtoto Na 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 13 inatamka waziwazi kuwa;
(1 ) Mtu hatamsababishia mtoto mateso, au aina nyingine ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto ikijumuisha mila na desturi zozote zenye madhara kwa mtoto kimwili au kiakili.
(2) Adhabu haitakuwa stahili kwa mtoto iwapo ni mbaya kwa aina yake au ni kubwa kwa kiwango chake kulingana na umri wa mtoto, hali ya mtoto kimwili na kiakili; na adhabu haitakuwa stahili kwa mtoto iwapo kutokana na umri mdogo wa mtoto au kwa sababu nyingine hawezi kuelewa lengo la adhabu hiyo. (3) Istilahi “udhalilishaji” kama ilivyotumika katika kifungu hiki maana yake kitendo kinachofanywa kwa mtoto kwa nia au dhamira ya kumdhalilisha au kushusha hadhi yake.
Kifungu Na. 14 inataja adhabu kwa mtu atakayekiuka kifungu chochote katika Sehemu hii atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja.
Pamoja na matamko mbalimbali yaliyotangulia kutolewa na viongozi na wanajamii kupinga kitendo kitendo cha utesaji na udhalilishaji kilichofanywa na waalimu hawa tarajiwa, Wizara inapinga na inalaani vikali shambulio hilo ambalo si tu limekiuka maadili ya utumishi wa umma hususani walimu lakini pia limevunja misingi yote ya haki za mtoto kama ilivyoelekezwa na Sera,Sheria na mikataba mbalimbali ya haki za mtoto ambayo nchi inatekeleza.Serikali inasistiza matumizi ya miongozo, raratibu na iliyopo katika kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watoto.
Serikali inapongeza wananchi wenye mapenzi mema na watoto kwa kutoa taarifa za matukio ya ukiukwaji wa haki za mtoto na kusihi kuendelea kufanya hivyo kwa maslahi bora ya mtoto.

Msemaji wa Wizara.

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO