MCDGC Publication

WIZARA YAANDAA MFUMO WA UFUATILIAJI WA SHUGHULI ZA WADAU WA MAENDELEO NA USATWI WA JAMII

WIZARA YAKUTANISHA WADAU KUPITIA MFUMO WA UFUATILIAJI WA SHUGHULI ZA WADAU WA MAENDELEO NA USATWI WA JAMII


Na Erasto Ching’oro- msemaji Wizara ya Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto.

Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa kikao kazi cha siku tatu kinachofanyika mkoani Morogoro kuhusu kuboresha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Shughuli za Maendeleo na Ustawi wa Jamii katika jamii.

Lengo kuu la mfumo utakaojadiliwa na wataam wa sekta ya maendeleo na ustawi wa jamii, ni kuwezesha wadau kuwa na mwongozo utakaotumika kupata mrejesho kuhusu utekelezaji wa Sera za maendeleo na ustawi wa jamii na kuhamasisha jamii kushiriki ipasavyo katika shughuli za kujiletea maendeleo na ustawi wa jamii. Aidha, mfumo unatachochea utendaji kazi, uwazi, uwajibikaji jamii miongoni mwa watendaji, na wasimamizi wa sera, mipango na mikakati ya maendeleo na huduma za ustawi wa jamii.

Aidha, Washiriki watapitia rasimu ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na SACCOs, VICOBA na vikundi vya kiuchumi kwa ajili ya kuimarisha uwezo wao kiuchumi.

Kikao hicho kimefunguliwa leo na Enterberth Nyoni, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara kuu ya Maendelo ya Jamii. Akifungua kiko hicho, Mgeni rasmi alieleza kuwa, ukamilishaji wa miongozo ya ufuatiliaji wa shughuli za wadau utaboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za Maendeleo na Ustawi wa Jamii kutoka kwa wadau mbalimbali na hivyo kutambua mchango wao kitaifa.

Maoni ya washiriki wa kikao kazi hicho cha siku mbili kianachofanyika Chuo cha Maendelo ya Wananachi Bigwa Mkoani Morogoro, yatasaidia kuzingatia ushiriki na uhamasishaji wa jamii katika utoaji, uhifadhi na uchambuzi wa taarifa za huduma za wadau katika maendeleo ya kisekta. Vile vile, Serikali itaweza kutambua shughuli zinazotekelezwa na wadau katika ngazi ya jamii, na kutathmini mchango wa wananchi katika kujiletea maendeleo yao.

Kaimu Mkurugenzi Entheberth Nyoni amaewahimiza wajumbe wa kikao kutafakari kwa makini namna bora ambayo Mfumo pendekezi utaweza kusaidiana na mifumo mingine iliyopo katika zoezi la ufuatiliaji na kutathmini ya miradi utekelezaji wa shughuli mbalimbli za kijamii.

Akitoa rai yake Kaimu Mkurugenzi, Nyoni, amebainisha kuwa kama Mfumo wa tathmini ya mchango wa wadau wa maendeleo na ustawi wa jamii utakamilika, utawezesha kuimarisha uratibu na usimamizi wa shughuli za maendeleo jamii katika ngazi ya Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kata na vijiji kwa ujumla.

Aidha, suala la mwongozo wa uanzishaji wa SACCOs, VIKOBA na kujiunga na vikundi vya kiuchumi, utasaidia kuwa na utaratibu wa pamoja wa uhamasishaji wa wanawake kujiunga na kuanzisha vikundi vya kiuchumi, kushirikiana na wadau na upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu maendelo ya vikundi.

Mkutano huo unahusisha washiriki kutoa Mashirika Yasiyo ya kiserikali, Wataalam wa Mendeleo na Ustawi wa Jamii kutoka katika ngazi za Wizara, OR TAMISEMI, Mikoa, Halmashauri, na serikali za mitaa. Kutokana na matarajio makubwa kwa wajumbe hao, Mgeni rasmi amehimiza wajumbe kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza tija katika utendaji wa Wizara husika. Akihitimisha nasaha zake, Nyoni ametoa wito kwa washiriki kutumia umahiri wao katika kuhakikisha ‘Mfumo wa shughuli za Maendeleo’ na ‘Mwongozo wa uundaji wa vikundi vya wanawake wajasiriamali’ kuona kuwa vinakidhi mahitaji ya sasa ya uratibu, usimamizi na kuimarisha utoaji huduma kwa jamii kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa maendeleo kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, ili wananchi waweze kupaa katika kujiletea maendeleo endelevu.