MCDGC Publication

WIZARA YAWATAKIA KHERI WATOTO WANAOANZA MTIHANI WA KUHITIMU KIDATO CHA NNE

TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUWATAKIA KHERI WATOTO WANAOANZA MITIHANI YA KUHITIMU KIDATO CHA NNE TAREHE 01 NOVEMBA, 2016

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kuwapongeza watoto wote wanaoanza kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya Sekondari kuanzia tarehe 01/11/2016. Wizara yenye dhamana kwa watoto inawatakia kheri na mafanikio watoto wote katika kufanya mitihani yenu, na tunaamini ya kuwa mmejiandaa vizuri. Ninawaomba mtambue kuwa hii ni fursa adhimu na hivyo ni lazima kuitumia vizuri kwa ajili ya mustakabali wa maisha yenu ya baadaye kwenu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

Nawaasa kuwa waangalifu muda wote wa kufanya mitihani, msikiuke taratibu na kanuni na pia msiandike vitu ambavyo havitakiwi katika makaratasi ya mitihani. Kipindi cha kufanya mitihani ni kifupi ukilinganisha na muda wa miaka minne mliotumia kukaa darasani na kusoma, hivyo mjiepushe na vishawishi vyovyote ikiwemo vitendo vya udanganyifu katika chumba cha mitihani ambavyo kwa namna moja au nyingine vinaweza kusababisha kufutwa kwa matokeo yenu na hivyo kukatisha ndoto zenu za kuendelea na masomo. Ni matarajio yangu kuwa wote mtamaliza mitihani yenu vizuri na kwa amani na utulivu.

Wakati watoto wetu wakiendelea kufanya mitihani yao, ninawaasa wazazi na walezi muelewe umuhimu wa siku hizi za mitihani, jitahidini kuwawekea watoto mazingira ya kuwawezesha kukumbuka yale waliyojifunza kipindi chote cha masomo yao na kuwa tayari kuyakabili mazingira ya mtihani kisaikolojia ili kufanya vizuri. Aidha Serikali haitarajii kusikia au kuona mzazi au mlezi yeyote akijaribu kuharibu au kutengeneza mazingira ya kuharibu ndoto ya mtoto yeyote hasa watoto wa kike kwa kupanga kumuozesha baada ya kumaliza elimu ya sekondari.

Kufanya hivyo ni kukiuka haki ya msingi ya mtoto ya kuendelezwa katika maisha yake, hivyo basi asiwepo mtu yeyote atakayethubutu kukatisha ndoto za watoto hawa. Serikali haitasita kuchukuwa hatua za kisheria kwa mzazi au mlezi atakayebainika kukiuka agizo hili kulingana na kanuni na sheria zinazomlinda mtoto.

Natoa rai kwa wazazi/walezi, makondakta wa mabasi na jamii kwa ujumla, tuwape ushirikiano watoto wetu hawa katika kipindi hiki cha mitihani yao ili waweze kufanya vizuri na kumaliza salama. Serikali yetu ipo katika harakati za kuelekea uchumi wa kati, hawa ni vijana wetu wanaotarajiwa kuendeleza taifa letu, hivyo tutoe kipaumbele katika kuwapa haki ya elimu ili kuwa na vijana mahiri waliondaliwa kubeba majukumu ya Taifa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki watoto wetu.

MARGARETH S. MUSSAI
KAIMU MKURUGENZI WA MAENDELEO YA WATOTO
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
31/10/2016